Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
UIMARISHAJI HUDUMA ZA MAJI MKURANGA, DAWASA YAPEWA MAUA YAKE
23 May, 2024
UIMARISHAJI HUDUMA ZA MAJI MKURANGA, DAWASA YAPEWA MAUA YAKE

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) mkoa wa kihuduma Mkuranga, imepongezwa kwa kuimarisha huduma ya maji kwa wananchi katika kitongoji cha Kiloweko,  kata ya Mipeko  katika Wilaya ya Mkuranga.

Kuimarika kwa huduma ya maji kumetokana na kukamilika kwa ufungaji wa Transfoma mpya katika chanzo cha maji Mwanambaya ambayo imesaidia kutatua changamoto ya uwepo wa  umeme mdogo (low voltage) na hivyo kupelekea kiwango cha  kusukuma maji kwa wananchi kuwa hafifu. 

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiloweko , ndugu Zaharani Ridhiwani  ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kutatua changamoto zinazohusu maji kwa wakati pale zinapojitokeza katika eneo lake.

"Tunashukuru Serikali na DAWASA kwa usikivu na uharaka wa kuendelea kuwajali wananchi, kipindi cha nyuma wananchi walikuwa wanapata shida ya maji kutokakana na changamoto ya umeme mdogo. Lakini DAWASA walipokea malalamiko hayo na kuyafanyia kazi na kwa sasa  wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika," aliongezea Ndugu Zaharani.

Naye Idd Madenge, mkazi wa Mwanambaya katika Kitongoji cha Kiloweko ameishukuru DAWASA-Mkuranga kwa kusikiliza kilio chao cha muda mrefu.

"Kukosekana kwa huduma  ya maji ya uhakika  katika makazi yetu ilikuwa ni changamoto ya muda mrefu, lakini kwa sasa tunaishuru serikali kwa kupitia  DAWASA imetatua kilio chetu cha muda mrefu, ni jukumu letu wananchi kutunza miundombinu  na vyanzo vya maji, pia naiomba DAWASA iendelee kuongeza huduma ya maji kwa maeneo ambayo bado ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji bora na salama," amefafanua.

Kwa upande wake msimamizi wa mradi , Mhandisi Richard Katwiga amesema  kufungwa kwa transfoma kumekuwa mkombozi kwa wananchi wa Mipeko na hivyo kuwasisitiza wananchi wanaohudumiwa na chanzo hicho kiendela kulinda miundombinu ya maji na kulipa ankara zao kwa wakati ili kusaidia upatikanaji wa huduma bora na endelevu. 

"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafanya jitihada nyingi katika kusogeza huduma kwa Wananchi  ikiwemo huduma ya maji, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kutambua jitihada hizi kwa kulinda miundombinu ya maji na kulipa ankara za maji wakati,” amesema.