UJENZI WA TANKI LA MAJI MSUMI WAFIKIA ASILIMIA 71.5, KUKAMILIKA JANUARI 2027
Ujenzi wa tanki kubwa la maji lenye ujazo wa lita 500,000 katika eneo la Msumi, Wilaya ya Ubungo, umefikia asilimia 71.5 ya utekelezaji, hatua inayodhihirisha maendeleo na juhudi za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) katika kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji kwa wananchi.
Mradi huo unaotekelezwa kwa kutumia fedha za ndani za DAWASA kwa gharama ya Shilingi milioni 996, unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Januari 2027 na kuwa suluhisho la kudumu la changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wapatao 22,370 wa maeneo ya Msumi na viunga vyake.
Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, Msimamizi wa Mradi, Mhandisi Aziz Namanga, amesema kuwa utekelezaji wa mradi umehusisha hatua tatu muhimu ambazo ni ujenzi wa msingi, usimikaji wa nguzo pamoja na tanki lenyewe la ujazo wa lita 500,000.
"Tunaendelea vizuri na utekelezaji wa mradi huu, na sasa tunaingia kwenye hatua muhimu ambayo inahusisha ujenzi wa tanki lenyewe la kuhifadhi maji, hivyo tunapambana sana ili kuhakikisha ifikapo mwakani mwezi januari tuwe tumemaliza na uanze kutoa huduma," amesema Mhandisi Namanga.
Aidha Mhandisi Namanga ameongezea kuwa mradi huo utekelezaji wake pia unahusisha ufungaji wa mabomba ya kuingiza na kusambaza maji kwa wananchi.
"Pia kwenye utekelezaji wa ujenzi wa tanki hili unahusisha ufungaji wa mabomba yenye ukubwa wa inchi 8 na inchi 12 yatakayoruhusu kuingiza na kutoa maji kwenye tanki na kupeleka kwa wananchi." amesema Mhandisi Namanga.
Nae mkazi wa Msumi Abubakari Mgeni, amepongeza DAWASA kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo, akisema unatoa matumaini mapya kwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji.
"Tunawapongeza sana DAWASA kwa kasi wanayoendelea nayo, tunaimani kukamilika kwa huu mradi basi sisi wakazi wa Msumi tunaenda kunufaika zaidi. Tumeona viongozi mbalimbali wamefika hapa kukagua hivyo inatupa moyo na imani kuwa kazi inaendelea vyema," amesema.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika mapema mwezi Januari 2027, ambapo tanki hilo litakuwa likipokea maji kutoka Kituo cha Kusukuma Maji cha Msumi na kuongeza uwezo wa kuhifadhi pamoja na kusambaza maji katika maeneo ya Msumi A, Msumi B, Msumi C na Tegeta A, hatua itakayoboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi, salama na ya uhakika kwa wakazi 22,370 wa maeneo hayo.
