VIJIBWENI HADI MJI MWEMA WAONGEZEWA WIGO WA HUDUMA ZA MAJI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inatekeleza mradi wa usambazaji Maji Maweni wenye lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa Kata za Vijibweni na Mjimwema Wilayani Ubungo
Mradi huo unategemea kukamilika Oktoba 2026 na unalenga kuhudumia jumla ya mitaa minne ambayo ni Mjimwema, Maweni, Ungindoni na Mkwajuni yenye wakazi takribani 800.
Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Ngusa Madaki amesema utekelezaji wa mradi unahusisha ulazaji wa mabomba yenye ukubwa wa inchi 8, 6 na 2, yenye urefu wa jumla ya kilomita 29 ambapo tayari Wateja 60 wameanza kunufaika na huduma ya Maji wakati ulazaji ukiwa unaendelea.
"Hadi sasa jumla ya kilomita 21.6 za mabomba zimeshalazwa kati ya kilomita 29.5 za mtandao wote wa mradi, na kazi ya uchimbaji na ulazaji wa mabomba inaendelea huku pia tukihamasisha wananchi kuendelea kuwasilisha maombi ya maunganisho ya huduma ya maji." amesema Mhandisi Ngusa
Ibrahim Kinjanga, mkazi wa Ungindoni, kata ya Mji mwema ameishukuru na kuipongeza DAWASA Kwa utekelezaji wa mradi huo ambao umeleta ahueni Kwa wakazi wa Mtaa huo
"Kwasasa ninapata maji baada ya utekelezaji wa mradi katika mtaa ninaoishi, nitoe rai Kwa wananchi wenzangu kuwasilisha maombi ya Huduma ili nao waweze kunufaika" amesema ndugu Kinjanga
