WAFANYABIASHARA WAJENGEWA UWEZO KUDHIBITI UPOTEVU WA MAJI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imewashirikisha wafanyabiashara wanaotumia maji katika shughuli zao, wakiwemo waosha magari, wafyatua matofali na watunza bustani, katika juhudi za kudhibiti upotevu wa maji na kulinda miundombinu.
Wafanyabiashara hao wamepewa elimu kuhusu matumizi sahihi ya maji, sheria na taratibu za huduma, pamoja na umuhimu wa kutoa taarifa mapema kuhusu uvujaji, uharibifu wa miundombinu au matumizi yasiyo halali ya maji.
Afisa Sheria wa DAWASA, Ezekiel Lwenge, amesema watumiaji wa maji wana wajibu wa kulinda miundombinu na kuzingatia sheria, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa wanapobaini uharibifu unaoweza kuathiri huduma.
“Ukiona uharibifu wa miundombinu ya maji, toa taarifa kupitia namba ya huduma kwa wateja 181 bila malipo, ambayo inapatikana muda wote,” amesema.
Kaimu Meneja wa Mkoa wa Kihuduma Temeke, Sufian Mvamila, amewataka wafanyabiashara kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya upotevu wa maji kwa kushirikiana na DAWASA.
“Mnapobaini uvujaji wa maji, uharibifu wa miundombinu, matumizi yasiyo halali au changamoto nyingine zinazoweza kuathiri huduma, toeni taarifa ili tuweze kutatua tatizo kwa haraka,” amesema.
Mfanyabiashara wa kuosha magari kutoka Azimio, Anzuruni Nuru, amepongeza ushirikishwaji wa wenyeviti wa mitaa katika kudhibiti upotevu wa maji, akisema wana nafasi ya kusaidia kubaini watu wanaoharibu au kutumia miundombinu kinyume cha sheria.
Naye mfanyabiashara wa kiwanda cha matofali kutoka Tandika, Jesca Kasebele, amesema elimu kuhusu sheria na matumizi sahihi ya maji imemsaidia kuelewa wajibu wake, ikiwemo umuhimu wa kuwa na vyombo vya kuhifadhi maji na kuyatumia kwa matumizi yaliyokusudiwa.
DAWASA inaendelea kuwashirikisha wafanyabiashara wanaotumia maji katika shughuli mbalimbali ili kuongeza uelewa, kulinda miundombinu na kupunguza upotevu wa maji.
