WAHUJUMU MIUNDOMBINU YA MAJITAKA WAONYWA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imewataka wananchi kuwa na matumizi sahihi ya miundombinu ya majitaka, kuepuka kutupa taka ngumu katika miundombinu hiyo na kuwa wa kwanza kutoa taarifa kwa anayeihujumu.
Imesema baadhi ya watu wanaohujumu miundombinu ya majitaka kwa kuiba mifuniko ya chemba za majitaka na kusababisha taka ngumu kuingia jambo linalosababisha kuziba kwa chemba na kutiririsha hovyo majitaka mtaani.
Mamlaka imesema hatua hiyo inahatarisha afya za wananchi kwa kuleta hatari ya kutokea magonjwa ya mlipuko kama kipindipindu.
Hayo yamesemwa na Mhandisi Mbaraka Mpala kutoka DAWASA, mara baada ya kushuhudia maboresho ya miundombinu ya majitaka katika mtaa wa Sinza A ili kuongeza ufanisi wa mifumo ya majitaka katika eneo hilo.
Mhandisi Mpala amesema eneo hilo lilikabiliwa na changamoto katika mifumo ya majitaka hali iliyosababisha kuziba kwa chemba na kutiririsha majitaka mtaani, jambo ambalo kwasasa wamelifanyia kazi na hali ni shwari.
"Katika mtaa wa Sinza A, tumefanya maboresho makubwa ya chemba za majitaka kwa kuzijengea vizuri na kuweka mifuniko imara ambayo itazuia taka ngumu kuingia katika mifumo iyo na kusababisha uzibaji," amesema Mhandisi Mbaraka.
Naye Mkazi wa mtaa wa Sinza A, Ndugu Haji Ally amepongeza hatua hiyo kwani utiririkaji majitaka mtaani kulisababisha kuhatarisha afya za wakazi wa eneo hilo hususani watoto wadogo.
"Ni jambo jema kazi hii imefanyika, chemba hizi kuwa wazi ilipelekea baadhi ya wananchi kutupa taka ngumu katika mifumo hiyo na kusababisha kuziba, majitaka yakiririka mtaani afya za watu zinakua hatarini kupatwa na magonjwa ukizingatia tuna watoto wadogo hapa mtaani," amesema Haji.