WAKAZI 502 KIJIJI CHA VIKUGE, KIBAHA WAFIKIWA NA HUDUMA YA MAJISAFI
Wananchi 502 wa Kitongoji cha Kigero, Kijiji cha Vikuge, Kata ya Soga, Wilaya ya Kibaha Vijijini, Mkoa wa Pwani wanatarajiwa kunufaika na huduma ya majisafi baada ya kuanza utekelezaji wa mradi wa Kigero.
Mradi huo una lenga kusogeza huduma ya maji kwa wakazi hao unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkoa wa Kihuduma Kibaha.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Msimamizi wa mradi, Mhandisi Emmauel Charles amesema kazi ya utekelezaji wa mradi imeanza kutoka kwenye chanzo cha bomba la inchi 8, na inahusisha ulazaji wa mabomba ya inchi 4, inchi 3 na inchi 2 ya kufikisha huduma kwa wananchi kikamilifu.
Amesema mradi unatekelezwa katika eneo la umbali wa kilomita 2 na unatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani kiasi cha Shilingi Milioni 29.2.
"Eneo hili ni mojawapo ya maeneo ambayo yamekuwa na changamoto ya huduma ya maji kwa muda mrefu na kutokana na uhitaji kuongezeka, imebidi tusogeze huduma ili kuwapunguzia usumbufu wa kutafuta na kununua maji maeneo ya mbali," amesema Mhandisi Charles.
"Kazi hii tunaifanya kwa bidii kubwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji haraka, tunatarajia kukamilisha mradi huu ndani ya wiki tatu na wananchi wataanza kupata huduma ya majisafi kikamilifu," amesema Mhandisi Charles.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Vikuge, Ndugu Richard Ngeleja ametanguliza shukrani zake na pongezi kwa DAWASA kwa kuwafikia na kuona hitaji lao kubwa la huduma ya majisafi katika eneo hilo lote.
"Wananchi wamekuwa wakipata shida sana ya namna ya kupata maji kwa urahisi, maji ambayo yamekuwa yakipatikana ni ya visima ambayo bado siyo salama sana kiafya, lakini tunashukuru leo tumeletewa mradi huu ambao tuna imani utakuwa suluhisho la tatizo letu hapa," ameeleza Ndugu Ngeleja.
Mkazi wa kijiji cha Vikuge, Ndugu Zaituni Issa ameomba mradi ukamilishwe kwa haraka kwani maji yamekuwa ya shida sana katika makazi yao, kwa kipindi kirefu wanatumia muda mwingi kwenda kuchota maji badala ya kufanya kazi zao nyingine za kijamii na kiuchumi.
