WAKAZI MATUGA WAPEWA ELIMU YA HUDUMA ZA MAJISAFI
Zaidi ya wakazi 300 wa Kitongoji cha Matuga, Kata ya Kawawa, Wilaya ya Kibaha Vijijini, Mkoa wa Pwani wameanza kunufaika na huduma ya majisafi na salama, baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa Matuga uliotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo katika eneo hilo.
Akizungumza katika kikao na wanufaika wa huduma hiyo, Afisa Huduma kwa Wateja DAWASA, Ndugu Grace Jason amewasisitiza wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya maji katika maeneo yao ili kuhakikisha huduma hiyo inakuwa endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Mamlaka inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma ya maji. Hivyo ni wajibu wenu kuilinda miundombinu hii ambayo imejengwa na kupita katika maeneo yenu,” amesema Ndugu Grace.
Aidha, amewahimiza wananchi wanaohitaji huduma ya maji kufuata taratibu rasmi kwa kuwasiliana na DAWASA ili kupata maunganisho mapya na huduma nyinginezo, badala ya kufanya maunganisho holela yanayokiuka sheria.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Matuga, Ndugu Geofrey Kazinduki, ameishukuru DAWASA kwa juhudi za kutekeleza mradi huo ambao umeleta matumaini mapya kwa wananchi wa eneo hilo.
Kwa upande wake, mkazi wa Kitongoji cha Matuga, Ndugu Zaituni Mwajuma amesema hapo awali walikuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji, hali iliyokuwa ikiathiri shughuli zao za uzalishaji na maendeleo ya familia lakini kupitia mradi huu, mambo yamebadilika na kila shughuli inafanywa kwa wakati.
Mradi wa maji Matuga umetekelezwa kwa kutumia fedha za ndani kiasi cha milioni 35.3 na umehusisha ulazaji wa mabomba ya inchi 3 na 2, kwa urefu wa kilomita 5 ili kuondoa changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji ambayo ilikuwa ikiwasumbua wananchi wa eneo hilo.
