WANAFUNZI MLIMANI WAKUMBUSHWA UMUHIMU WA KUTUNZA MIUNDOMBINU YA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea kutoa elimu katika klabu za maji na usafi wa Mazingira katika shule ya msingi Mlimani iliyopo Wilaya ya Ubungo na kusisitiza juu ya umuhimu wa utunzaji wa miundombinu ya maji.
Shule hiyo ni miongoni mwa shule 10 za Mazingira zinazosimamiwa na kuendeshwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Afisa Mawasiliano kutoka DAWASA Bi. Hashura Kamugisha ameeleza shughuli (tabia) mbalimbali zinazopelekea uharibifu wa miundombinu ya maji pamoja na hatua za kufuata pale uharibifu wa miundombinu ya maji inapokuwa imeharibiwa katika maeneo yao.
"Huduma ya majisafi inategemea sana ulinzi wa miundombinu ya maji, hivyo ili kuhakikisha tunaendelea kunufaika na huduma ya maji ni wajibu wa kila mmoja kutunza miundombinu ya maji katika maeneo yenu mnayoishi"ameeleza Ndugu Kamugisha.
Nae Mwalimu Mwanzo Lazaro mlezi wa klabu ya mazingira shuleni hapo ameishukuru Mamlaka kwa jitihada za kutoa elimu ya utunzaji wa miundombinu ya maji kwa wanafunzi na kusisitiza juu ya utunzaji wa miundombinu ya maji katika maeneo wanayoishi au ikiwemo katika mazingira ya shule.
"Elimu ya utunzaji wa miundombinu ya maji ni elimu inayopaswa kurithishwa kwa watu wa rika zote, kuanza na hawa wanafunzi wadogo kunawasaidia kujijengea tabia endelevu na kuchukua majukumu ya utunzaji wa miundombinu ya maji. Msisitize kutoa taarifa pindi mtakapoona unapotokea mkiwa nyumbani au hata shuleni" ameeleza Mwl. Lazaro.
Mwanafunzi Khadija Mustapha ambae ni mwanachama wa klabu ya maji na usafi wa Mazingira ya shule ya msingi Mlimani ameishukuru DAWASA kwa kuwa mlezi na kutoa nafasi ya wao kujifunza mambo mbalimbali ya Maji na Usafi wa Mazingira na kuomba nafasi ya kuendelea kujifunza kwa vitendo ili kufahamu zaidi namna Mamlaka inavyoendelesha shughuli zake.
Mamlaka inasaidia kuelimisha vijana kuhusu utunzaji wa miundombinu ya maji ili wajenge uwezo na uelewa mkubwa wa maswala ya maji na usafi wa Mazingira, pia imejikita katika kuhakikisha inafikia wanajamii wa rika zote na kutoa elimu, kwani inaamini mabadiliko ya kitabia yanachangia kuwepo kwa utamaduni mzuri wa kuhifadhi miundombinu ya majisafi na majitaka na wanafunzi ni mabozi wazuri katika jamii.