Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
WANAFUNZI ZANAKI WAPEWA DARASA UTUNZAJI MAZINGIRA
26 Jul, 2025
WANAFUNZI ZANAKI WAPEWA DARASA UTUNZAJI MAZINGIRA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imewasisitiza wanafunzi wa Shule ya Sekondari Zanaki kuendelea kuhifadhi mazingira ili kuwawezesha kujifunza kwa ufanisi.

Zanaki iliyopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa shule 11 za mazingira zinazosimamiwa na kuendeshwa na DAWASA. Pamoja na mambo mengine, wanapewa elimu ya kutunza mazingira, matumizi sahihi ya maji na kulinda miundombinu ya majisafi.

Afisa Mawasiliano kutoka DAWASA, Husna Richard ameelezea umuhimu wa usafi wa mazingira shuleni na maeneo yote yanayowazunguka huku akisisitiza utunzaji sahihi wa taka shuleni katika kuhakikisha shule na mazingira yanakuwa sehemu salama ya kujifunza muda wote.

"Mazingira safi na salama huchochea hali ya kujifunza, yana mchango mkubwa katika kufanya masomo kuwa ya kuvutia zaidi na ni muhimu kwa afya ya akili kwani huepusha magonjwa katika mazingira yetu," amesema Husna.

Mara baada ya mafunzo hayo, Mwalimu Esther Swai ambaye ni mlezi wa klabu ya mazingira shuleni hapo, ameishukuru DAWASA kwa jitihada za kuwafikia watoto wa shule za msingi na sekondari na kutoa elimu ya maji na usafi wa mazingira akiamini itakuwa chachu ya mabadiliko kwa vijana hao.

"Elimu ya maji na usafi wa mazingira ni elimu inayorithi kizazi na kizazi kwakuwa inalenga mabadiliko ya kitabia hivyo tunaishukuru sana DAWASA kwa jitihada za kutoa elimu hiyo kwa vijana wetu hakika ni hazina ya kudumu," amesema Mwlimu Swai.

Mwanafunzi Warda Jihadhari ambaye ni mwanachama wa klabu ya maji na usafi wa Mazingira shuleni hapo ameishukuru DAWASA kuwa mlezi na kutoa nafasi ya wao kujifunza mambo mbalimbali ya maji na usafi na kuomba nafasi ya kuendelea kujifunza kwa vitendo ili kufahamu zaidi namna Mamlaka inavyoendesha shughuli zake.

"DAWASA imekuwa mlezi wa klabu yetu ya mazingira kwa muda sasa na kila mara tunajifunza vitu mbalimbali kuhusu Majisafi na Usafi wa Mazingira. Elimu ya leo imesaidia kujenga uelewa zaidi kuhusu matumizi sahihi ya maji hasa kwa sisi wanafunzi ili kuweza kupunguza gharama kubwa ya bili za maji na kuendelea kupata huduma ya maji endelevu," amesema Jihadhari.

Mamlaka inasimamia klabu za mazingira shuleni kwa kutoa elimu mbalimbali kuhusu Majisafi na Usafi wa Mazingira, utunzaji wa miundombinu ya maji pamoja na vyanzo vya Maji na kuwaandaa wanafunzi katika rika lao kuwa mabalozi wema katika jamii katika masuala yote yanayohusu maji.