WATEJA ILALA WASISITIZWA KUZINGATIA USOMAJI, UHAKIKI DIRA ZA MAJI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkoa wa Kihuduma Ilala imeendelea kuwakumbusha wateja juu ya umuhimu wa usomaji na uhakiki wa mita mara baada ya kupokea ujumbe wa usomaji mita kwenye simu zao ili kuongeza uwazi na ufanisi katika utoaji huduma.
Akizungumza, Afisa Ankara wa DAWASA Ilala, Ndugu Magreth Anyimike amesema zoezi la usomaji mita ni shirikishi na linafanyika sambamba na uhakiki wa usomaji ambapo wateja wanapata nafasi ya kuhakiki mita zao kabla ya kuandaliwa bili za mwezi.
"Zoezi la usomaji mita bado linaendelea na baadhi ya wateja wameanza kupokea jumbe fupi za uhakiki wa usomaji, tunawakumbusha wateja wetu ni muhimu kuhakiki usomaji mita na kutoa taarifa kama kuna changamoto ili tuifanyie kazi kwa wakati.
Taarifa hizo zinapokelewa kupitia namba ya huduma kwa Wateja 181(bure), mitandao ya kijamii au wafike katika ofisi zetu kwa msaada zaidi," amesema Ndugu Magreth.
Ndugu Magreth, amesisitiza ushirikiano kati ya wateja na Mamlaka ni muhimu kwani unaboresha utendaji kazi wa watumishi kwa kutoa huduma bora.
Mkoa wa Kihuduma DAWASA Ilala una jumla ya wateja takribani 17,504 na unahudumia Kata za Ilala, Mnyamani, Kivukoni, Jangwani, Mchafukoge, Mchikichini, Kisutu, Gerezani, Upanga Magharibi na Upanga Mashariki.
