WATUMISHI DAWASA WAKUMBUSHWA KUZINGATIA SHERIA UTOAJI HUDUMA KWA WANANCHI

Watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) wameaswa kuzingatia uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa mahali pa kazi ili kuboresha huduma kwa wateja na kuleta tija kwa Serikali.
Hayo yamesemwa na Afisa Mchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Bi Janeth Kafuko wakati wa Semina ya kuwajengea uzoefu na maadili ya Utumishi wa Umma ikiwemo kuepuka vitendo vya Rushwa.
Amewaeleza Watumishi kuwa ni kosa la jinai kwa Mtumishi wa Umma kujihusisha na vitendo vya udanganyifu ili kujipatia fedha isiyo halali, ikiwemo kumrubuni mteja ili kupata fedha.
"Kila mmoja anatakiwa kutekeleza majukumu yake aliyopewa na kiongozi wake na sio nje ya hapo, kwa kuwa kufanya kazi nje ya utaratibu ndiko kunakosababisha kuwepo kwa vitendo vya udanganyifu na mianya rushwa," amesema Bi Janeth.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja DAWASA CPA Rithamary Lwabulinda amesema kuwa kada ya Watumishi wanaosoma mita za Maji ni nguzo muhimu kwa Taasisi kwa kuwa hukutana na wateja moja kwa moja katika utendaji wao wa kila siku.
"Watumishi wa kada hii ni kundi muhimu sana na lenye kutegemewa na Taasisi, hivyo mnapaswa kuzingatia nidhamu katika kuwahudumia wateja kwa kulinda taswira ya Taasisi ili wateja mnaowahudumia waridhike na huduma," amesema Rithamary.
Vilevile amewakumbusha kutokujihusisha na vitendo viovu vya uhujumu wa miundombinu ya maji pamoja na kuwarubuni wateja kwa lengo la kujipatia fedha zisizo za halali kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Nae Calvin James, Mtumishi wa DAWASA Kawe amesema mafunzo hayo inawasaidia kuwapa ujuzi kwa wa kutosha katika utendaji wao wa kazi na kuwapa miongozo sahihi ya utumishi wa umma.
"Semina hii imetusaidia sana kujua namna bora ya utendaji kazi zetu na imetupa kujua sheria na taratibu zilizopo katika utumishi wa Umma," amesema.