Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
WAZIRI AWESO ARIDHISHWA NA MIKAKATI YA DAWASA KUELEKEA EL NINO
25 Sep, 2026
WAZIRI AWESO ARIDHISHWA NA MIKAKATI YA DAWASA KUELEKEA EL NINO

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amefanya ziara ya kukagua miundombinu ya maji inayosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa lengo kwa lengo la kubaini usalama wa miundombinu hiyo na utayari wa Mamlaka kuelekea katika kipindi cha mvua kubwa za El Nino zinazotarajiwa kuanza mwezi wa kumi mwaka huu. 

Hatua hiyo imekuja kufuatia tahadhari ya uwepo wa mvua kubwa za El Nino zinazotarajiwa kuanza kunyesha kutolewa na Mamlaka ya Hali ya hewa Nchini (TMA)

"Tumefanya ukaguzi maeneo mbalimbali ya kihuduma DAWASA kwa kuanzia eneo la Mpiji ambalo liliwahi kupatwa na changamoto ya kuharibika wakati wa mvua, na tumejionea kazi inayofanywa na DAWASA ya kuboresha ulinzi katika miundombinu hiyo, pia tumejionea kazi inayofanywa ya kuboresha huduma ya usafi wa mazingira katika makazi ya wananchi ili kuepusha uchafuzi unaoweza kujitokeza hasa kwa wananchi wenye tabia ya kutiririsha majitaka barabarani," amesema Mhe. Aweso. 

"Kazi inayofanyika inaonesha namna Mamlaka ilivyojipanga na kujiandaa dhidi ya mvua hizi za muda mrefu," ameeleza. 

Ameziagiza Mamlaka zote za Maji Nchini kuweka mikakati madhubuti ya namna ya kuhakikisha pale panapotokea maji yamechafuka katika vyanzo vya maji kutokana na mvua wanakuwa na utaratibu wa kuyatibu ili kuhakikisha maji yanayotolewa yanakuwa safi na salama kwa matumizi ya wananchi. 

"Pia Mamlaka zihakikishe zinaunda vikosi kazi vya kufuatilia changamoto za huduma pale zinapotokea katika kipindi cha mvua," amesisitiza Waziri Aweso. 

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa tayari Mamlaka imeshabaini maeneo takribani 21 ya miundombinu ya maji ya kuyawekea ulinzi ili kukabiliana na mvua zitakazoanza kunyesha. 

Amesema pia kuwa, Mamlaka imeanzisha vituo sita vya kusambaza vifaa vya kuboresha miundombinu ya maji ikiwa ni pamoja na mabomba kipindi cha mvua kama miundombinu itapata changamoto ya kufikiwa.

Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Mamlaka na Serikali kwa kuacha kufanya shughuli za uchimbaji wa mchanga katika vyanzo ya maji ili kulinda usalama wa miundombinu ya maji iliyopo.