Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
WAZIRI AWESO ASISITIZA DAWASA KUWA NA UONGOZI WA MIKAKATI NA TIJA
25 Feb, 2026
WAZIRI AWESO ASISITIZA DAWASA KUWA NA UONGOZI WA MIKAKATI NA TIJA

Waziri wa Maji, Mhe.Jumaa Aweso (Mb), amekutana na viongozi waandamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)  ambapo amewataka kuwa na uongozi wa kimkakati na ufanisi katika utoaji wa huduma huku akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, weledi na ubunifu katika kuimarisha huduma za maji safi na salama kwa wananchi.

Katika kikao hicho, Mhe.Aweso ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, mhandisi Mwajuma Waziri, Naibu Katibu Mkuu, ndugu Rose Ambrose pamoja na Viongozi na Watendaji wa Wizara ya Maji.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, mhe. Aweso amesema kuwa viongozi waandamizi wana jukumu la kuhakikisha DAWASA inaweka mipango inayoendana na dira ya Taifa ya mwaka 2050 na kuisimamia ili kuleta mapinduzi katika utoaji wa huduma ya Maji.

“Ninyi mkawe viongozi wenye uwezo wa kufanya tathmini thabiti, kupanga kimkakati na kusimamia rasilimali na kuwajibika kikamilifu kwa matokeo. Wananchi wanatarajia huduma bora, na hilo linawezekana kupitia uongozi thabiti na wenye maono,” alisema mhe. Aweso.

Mhe. Aweso ameongeza kuwa Wizara ya Maji itaendelea kuwekeza katika kujenga uwezo wa watumishi ili kuongeza tija, kuimarisha mifumo ya usimamizi wa miradi ya maji, na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika.

Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa kikao hicho kimelenga kuwajengea viongozi uelewa wa kina juu ya uongozi wa kimkakati, maadili ya utumishi wa umma, pamoja na mbinu za kuongeza uwajibikaji na uwazi katika utendaji wa taasisi.

"Mafunzo haya yanatarajiwa kuleta matokeo chanya katika kuboresha huduma kwa wateja, kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa miradi ya maji, na kuimarisha utamaduni wa uwajibikaji miongoni mwa viongozi waandamizi wa mamlaka hiyo, hiki ndicho tunacholenga" amesema mhandisi Bwire