WAZIRI WA MAJI ATETA NA WENYEVITI SERIKALI ZA MITAA DAR UIMARISHAJI HUDUMA YA MAJI
Waziri wa Maji, Mhe.Jumaa Aweso (Mb) amekutana na kuzungumza na Viongozi wa Wenyeviti wa Serikali za mitaa kutoka Wilaya 5 za mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Menejimenti ya DAWASA ikiwa ni muendelezo wa jitihada za kupweka mipango ya pamoja pamoja na kupata suluhu ya upungufu wa Maji katika mkoa wa Dar es Salaam iliyochangiwa na mabadiliko ya tabia ya nchi na kuathiri uzalishaji.
Mhe. Aweso amewashukuru Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Kwa kushirikiana na Watendaji wa DAWASA haswa katika utoaji wa taarifa kuhusu hali ya Maji na kurahisisha utoaji wa Huduma Kwa wananchi kwani viongozi hao ndiyo wako katika maeneo hayo yanayotegemea Huduma kutoka DAWASA.
"Niwashukuru sana kwa jitihada mnazoendelea kufanya za kuwataarifu wananchi juu ya changamoto hii tunayopitia pamoja na upatikanaji wa maji kupitia mgao, siku zote nimekua nikisema Jamii ipo na ili tufanikiwe ni lazima tuwashikirishe katika shughuli zetu, niwashukuru Kwa kazi kubwa mnayoendelea kuifanya" ameeleza Mhe.Aweso.
Waziri Aweso amesisitiza kuendelea kuwepo kwa ushirikiano wa karibu baina ya DAWASA na Wenyeviti wa Serikali za mitaa ambapo ameelekeza DAWASA kudumisha Uhusiano na Wenyeviti hao ili kubaini changamoto katika Mitaa pamoja na kuwashirikisha mipango iliyopo katika uimarishaji wa Huduma.
Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire ameahidi kushirikiana bega Kwa bega na Viongozi hao ikiwemo kusaidiana katika kufuatilia Migao pamoja na kuainisha maeneo yenye Visima katika Mitaa ambavyo vinaweza kuwekwa kwenye mfumo wa usambazaji Maji ili kuongeza Kiwango Cha maji yanayosambazwa Kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar Es Salaam, ndugu Juma Mwindamno ameeleza kuwa wanaenda kufanyia kazi maadhimio waliofikia na DAWASA ikiwa ni pamoja na kufikisha taarifa za visima vyote vilivyopo katika mitaa yao ili viweze kufuatiliwa na kuboreshwa. Hatua itakayosaidia wananchi kupata huduma ya maji katika kipindi hiki cha mpito na kuahidi ushirikiano wa kutosha kwa DAWASA.
"Tunawashukuru DAWASA Kwa kutushirikisha katika mipango ya kutatua hali hii ya upungufu wa Maji, tuna ahidi tutaendelea kutoa ushirikiano ili tuvuke Kwa pamoja".ameeleza ndugu Mwindamno
