WIZI WA MITA ZA MAJI WAMFIKISHA DAUDI KORTINI
Daud George, Mkazi wa Kinondoni Jijini Dar es salaam amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka matatu ya uhujumu uchumi ikiwemo la kuiba mita za maji na kuisababishia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) hasara ya takribani shilingi laki tisa (900,000)
Wakili wa Serikali, Erick Kamala akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki amesema ndugu Daudi anashtakiwa kwa kuharibu miundombinu ya kutoa huduma muhimu, kuiba mita tatu za maji mali ya DAWASA pamoja na kusababisha hasara ya takribani shilingi laki tisa kwa Mamlaka hiyo.
Mshtakiwa anadaiwa kutenda makosa hayo mnamo Novemba 18, 2024 katika eneo la Sindano, Mwananyamala linalohudumiwa na Mkoa wa kihuduma DAWASA Kinondoni.
Hakimu Beda Nyaki amehairisha kesi hiyo hadi tarehe 21 Januari 2025 itakapotajwa ambapo mshtakiwa amerudishwa rumande.
DAWASA inawakumbusha Wananchi kuwa Sheria ya Maji Namba 5 ya mwaka 2019 kifungu cha 61 kinasema ni kosa kuharibu miundombinu ya Majisafi au Majitaka au mali ya Mamlaka na faini yake ni kiasi kisichopungua milioni tano na kisichozidi milioni hamsini au kifungo cha miaka miwili hadi mitano.