Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
ZAIDI YA WAKAZI 200 KUNUFAIKA NA MAUNGANISHO YA MAJI PWANI
13 Aug, 2024
ZAIDI YA WAKAZI 200 KUNUFAIKA NA  MAUNGANISHO YA MAJI PWANI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendesha zoezi la utoaji wa vifaa vya maunganisho mapya ya maji kwa wakazi 200 wa maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani. 

Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji wa vifaa hivyo, Meneja wa Mkoa wa Kihuduma Kibaha Ndugu Alpha Ambokile ameeleza kuwa kwa sasa Mamlaka imekuja na utaratibu wa kufikisha vifaa vya maunganisho ya maji majumbani kwa wateja na kuwakabidhi pamoja na kuwaunganishia huduma papo kwa hapo. 

Amesema kuwa wateja waliokabidhiwa vifaa ni kutoka Kata ya Msangani, Kongowe, Mkuza, Mailimoja, Visiga na Zegereni. 

"Kwa upande wa Pwani tumekuja kitofauti na mfumo uliokuwa awali, kwa sasa vifaa vya maunganisho mapya vinawafuata wananchi majumbani mwao na baada ya kukabidhiwa mwananchi anaunganishwa na huduma wakati huohuo, lengo ni kumpa nafasi mteja ya kupata huduma kwa haraka," ameeleza na kuongeza mfumo huu pia unaisaidia Mamlaka kutekeleza maunganisho ya maji kwa wananchi kwa wakati na kwa uhakika Ndugu Ambokile," amesema. 

Ameongeza kuwa katika Mkoa wa Pwani kuna wateja zaidi ya 800 waliokuwa wameomba kupata huduma ya majisafi na kwa leo tumefanikiwa kuwaunganisha wateja 130 na huduma ya majisafi. Zoezi litaendelea mpaka likamilike kwa wateja wote. 

"Maombi ya maunganisho ya huduma ya majisafi yalikuwa ni mengi, lakini tunashukuru kwa kuanza zoezi hili ambalo kwa leo wateja 200 tayari wamepata vifaa na huduma ya maji imewafikia, hii ni hatua endelevu ya Mamlaka ya kufikisha huduma bora kwa kila mwananchi na huduma inakuwa bora.

Ndugu Ambokile amewakumbusha na kuwahimiza wananchi ambao wamepokea vifaa vya maunganisho mapya kutunza miundombinu ya Maji, kutumia huduma ya Maji kwa usahihi na kulipia bili za maji kwa wakati ili kuiwezesha Mamlaka kutoa huduma endelevu.

Mtendaji wa Mtaa wa Galagaza Bi. Sarah Pongone ameishukuru sana Mamlaka kwa kufikisha huduma hii mtaani na kuwataka wananchi kutunza miundombinu ya maji vizuri. 

Ndugu Swaum Juma mkazi wa mtaa wa Galagaza ameishukuru sana DAWASA ukiachana na kuniletea na kunikabidhi vifaa, wamehakikisha kuwa bomba langu linatoa maji.