ZANAKI WAPEWA ELIMU YA KUDHIBITI UPOTEVU WA MAJI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa elimu kuhusu umuhimu wa maji, udhibiti wa upotevu na utunzaji wa miundombinu ya maji kwa wanafunzi wa Klabu ya Mazingira ya Shule ya Sekondari Zanaki, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.
Elimu hiyo imelenga kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu umuhimu wa kutunza rasilimali ya maji na miundombinu yake, ili wawe mabalozi wa huduma hiyo muhimu katika familia na jamii zao. Akizungumza wakati wa kutoa elimu hiyo, Afisa Mawasiliano wa DAWASA, Prisca Makenya, amesema maji ni rasilimali muhimu kwa binadamu, wanyama na mimea, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuyatunza na kulinda miundombinu inayowezesha upatikanaji wake.
“Utunzaji wa miundombinu ya maji ni muhimu kwani unapunguza gharama zinazojitokeza wakati wa uharibifu na unasaidia kuhakikisha wananchi wanapata majisafi na ya uhakika,” amesema Makenya.
Amesema klabu za mazingira mashuleni ni sehemu ya mkakati wa kuwajengea vijana uwezo kuhusu maji na usafi wa mazingira, ili wawe chachu ya mabadiliko na mabalozi wa kulinda huduma hiyo katika jamii. Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Zanaki, Damian Baraza, ameishukuru DAWASA kwa kutoa elimu hiyo na kuwataka wanafunzi kuitumia kwa kuhamasisha jamii kutunza miundombinu na kutoa taarifa za uharibifu wa mabomba kupitia namba 181 bila malipo.
Naye mwanafunzi Warda Jihadhari ameishukuru DAWASA kwa elimu hiyo, akisema imewasaidia kuelewa umuhimu wa kulinda miundombinu na kuchukua hatua wanapoona upotevu wa maji.
Ameahidi kwa niaba ya wanafunzi wenzake kuwa mabalozi wazuri wa kampeni hiyo, huku akiwahimiza wananchi kulinda miundombinu na kulipa bili za maji kwa wakati. Klabu ya Mazingira ya Shule ya Zanaki ni miongoni mwa klabu 12 zinazosimamiwa na DAWASA katika Dar es Salaam na Pwani kwa lengo la kuwajengea vijana uelewa na kuwashirikisha katika utunzaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira.
